Waziri asimamisha likizo za Marubani ATCL


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaak Kamwelwe, amesimamisha likizo za marubani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) katika kipindi cha mwisho wa mwaka.

Amesema marubani wa ATCL ambao wameshaanza likizo wanapaswa kurudi kazini na kuendelea na kazi ya kutoa huduma kwa wananchi.

Kamwelwe aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea mkoani Mbeya kwenye ukaguzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe (SIA).

Alisema wafanyakazi wa Mamalaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) nao hawapaswi kwenda likizo kipindi hiki cha mwisho wa mwaka bali wanapaswa kuhakikisha magari yaendayo mikoani hayapandishi nauli.

"Hakuna Mtanzania atakayepata shida ya kusafiri kipindi hiki cha sikukuu. Tumejipanga kusafirisha abiria hadi usiku," alisema Waziri Kamwelwe.

Alisema maofisa wa Sumatra wanapaswa kuhakikisha abiria hawaonewi wala kusumbuliwa na wenye mabasi hususani eneo la Ubungo ambalo limekuwa na walanguzi wengi wa tiketi.

"Kipindi hiki cha mwisho wa mwaka wananchi wengi wanataka kwenda kupumzika mikoani baada ya kufanya kazi kwa mwaka mzima pia ukizingatia Shirika la Ndege la FastJet limesitisha safari zake nchini, hivyo kutakuwa na uhaba wa ndege. Sasa naagiza marubani wote hakuna kwenda likizo, wahudumie wananchi, " alisema Waziri Kamwelwe.

Alisema katika kuhakisha ATCL inahudumia wananchi vizuri, baadhi ya viwanja vya ndege vikiwamo cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na Mwanza vyenye taa, ndege za ATCL zitakuwa zinafanya safari zake saa 24.

Alisema kiwanja cha ndege cha Songwe bado kiko katika matengenezo na kwamba mkandarasi anayejenga njia ya kutua ndege anapaswa kurudia ujenzi huo kutokana na kujenga chini ya kiwango.

Aidha, Waziri Kamwelwe aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuhakikisha wanatengeneza viyoyozi vilivyoko eneo la JNIA kwa kuwa havifanyi kazi muda mrefu na kusababisha kero kwa abiria.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela, alisema watayashughulikia maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Kamwelwe.

Comments

Popular posts from this blog

Wapinzani: Spika tengua kauli yako

Kitakachojiri katika mabasi Des. 20