Nyumba zaidi ya 300 zimezama na maji baada ya kukumbwa na mafuriko
katika Kata ya Magaoni, hivyo kusababisha wakazi wake kuhama makazi yao.
Tukio lilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 7:00 usiku baada ya mvua kubwa kunyesha usiku kucha.
Mwenyekiti wa Kata ya Magaoni, Kassim Abdallah, ambaye pia nyumba yake
imezama, alisema kuwa mvua iliyonyesha usiku wakuamkia jana, imeacha
hasara kubwa kwa wakazi wa kata hiyo kutokana na kuzingirwa na maji,
huku mali mbalimbali zikiharibika.
Alisema mvua hiyo ilianza kunyesha wakati huo mpaka saa 2:00 asubuhi,
hivyo kusababisha idadi kubwa ya wananchi kukosa mahali pa kuishi, hivyo
kuhamia katika shule na wengine kuhifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao.
Abdallah alisema kata hiyo ni mpya kwa kuwa mwanzo ilikuwa sehemu ya kata ya Mabawa kabla ya kugawanywa.
Alisema sababu kubwa ya mafuriko hayo ni kukosekana kwa mifereji ya
kutosha, hivyo kushindwa kuruhusu maji kutiririka kwa urahisi.
Mwenyekiti huyo alisema Diwani wa Kata hiyo, Mohamed Rajabu, baada ya
kuchaguliwa mwaka 2015 alijitahidi kuhakikisha mifereji inajengwa
lakini iliyopo haitoshelezi mahitaji ndiyo maana imekuwa rahisi kutokea
mafuriko.
Kutokana na athari hiyo, aliiomba Halmashauri ya Jiji la Tanga kutenga
fedha kwa ajili ya mifereji, vinginevyo maafa yanaweza kuwa makubwa
zaidi.
Naye Diwani Rajabu alisema mvua hiyo imesababisha mafuriko makubwa na
kwamba mpaka sasa wananchi hawana mahali pa kuishi na wamezikimbia
nyumba zao huku vyombo vyote vikiwa vimeharibika.
Alisema kuwa ili kuondoa tatizo hilo, alisema ni lazima Halmashauri ya
Jiji la Tanga ipange bajeti kwa ajili ya kutengeneza mifereji
ya kupitisha maji katika kata hiyo, vinginevyo kunawezekana kutokea
maafa makubwa zaidi.
Comments