Krismasi yatisha bei ya vyakula,nguo
WAKATI watu wakiendelea na maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, bei za bidhaa mbalimbali katika masoko na maduka zimeanza kupanda.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA katika baadhi ya maduka na masoko yaliyoko katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma umebaini baadhi ya bidhaa kama nguo na vyakula zimeanza kupanda.
Mmoja wa wafanyabiashara wa nguo na viatu katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, Joseph Erasto, alikiri baadhi ya bidhaa zimepanda bei kwa sababu msimu wa sikukuu huwana wateja wengi.
“Bei zinapanda wakati wa sikukuu kwa sababu kuna kuwa na wateja wengi tofauti na wakati mwingine, ndiyo maana wafanyabiashara hutumia fursa hiyo,” alisema Erasto.
Katika baadhi ya maduka ya nguo za watoto bei ya nguo za daraja la chini kwa watoto wa kike zilikuwa kati ya Sh 25,000 na 35,000 wakati kwa nguo za kati na juu ilikuwa kuanzia Sh45,000 hadi Sh 95,000.
Hata hivyo wamachinga walionekana kuwa kimbilio kubwa kwa wateja mbalimbali waliofika kupata mahitaji yao.
Mmoja wa wa kaziwa Temeke, Dar es Salaam, Anna Riwa ambaye alikutwa akichagua nguo za watoto kwa machinga, alisema kuna unafuu wa bei kulinganisha na madukani.
“Mimi nimeanzia kuzunguka madukani lakini nimeshindwa kununua nguo ya mwanangu, unauliza gauni unaambiwa Sh 35,000 lakini ukija kwa machinga gauni hilo hilo unanunua kwa Sh28,000,” alisema Anna.
Kwa upande wa vitoweo, mbuzi katika machinjio ya Vingunguti alikuwa akiuzwa kati ya Sh 80,000na Sh 150,000.
Mmoja wa wafanyabiashara wa mbuzi katika eneo hilo, Baraka Adam, alisema biashara katika msimu huu inaridhisha.
“Hata kwa Sh 60,000 au 75,000 unaweza kupata mbuzi lakini kama unataka wa kiwango kama huyu (anamuonesha mwandishi) tunauza Sh 80,000,” alisema Adam.
Baadhi ya wafanyabiashara waliwashauri wateja kujenga utaratibu wa kununua mapema bidhaa kama nguo badalaya kusubiri hadi wakati wa sikukuu.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Abdallah Mwinyi, alisema biashara si nzuri ingawa haiwezi kufanana na miezi ya nyuma.
“Biashara si nzuri japo haiwezi kufanana na ilivyokuwa Aprili, kuna tofauti lakini si kama tulivyokuwa tumetegemea,” alisema Mwinyi.
Alisema kuchelewa kutolewa kwa mizigo bandarini kulisababisha wafanyabiashara wengi kukosa bidhaa kwani mizigo iliyokuwa iingizwe sokoni Oktoba ilikwama hadi Jumamosi iliyopitandiyo ilianza kutolewa.
“Mizigo ilichelewa kutolewa kwa sababu ya taratibu za TBS (Shirika la Viwango),wafanyabiashara wengine walitoka mikoani kuja kufuata mizigo Dar lakini wakakosa,”alisema.
Alisema mizigo inayoingia sokoni hivi sasa haitauzika kwa kiwango walichotarajia na kushauri TBS iongeze mawakala wa ukaguzi nje ya nchi na ikiwezekana iruhusu mizigo iingizwe na kuja kukaguliwa nchini.
“Mitaji itakatana bidhaa zitalala, tuboreshe sheria kumrahisishia mfanyabiashara kuingiza bidhaa nchini na Mtanzania apate kwa gharama nafuu,” alisema.
Kuhusu bei zabidhaa kuwa juu, alisema suala hilo halimuhusu mfanyabiashara na kudai kuwa sheria za kodi ndizo zinasababisha kusiwe na utulivu wa bei sokoni.
MTAA WA KONGO
Katika mtaa maarufu wa Kongo uliopo eneo la Kariakoo, Dar es Salaam kulikuwa napilika pilika za watu kufanya manunuzi ya nguo na mahitaji mengine.
Mbali ya mtaa huo kulikuwa na msongamano wa watu na magari katika mitaa mingine ya Kariakoo hatua iliyosababisha kupitika kwa tabu.
Baadhi ya wanawake walionekana kuchukua tahadhari kubwa huku wakiwa wamekumbatia mikoba yao tumboni na wengine wakiinyanyua juu.
JIJINI DODOMA
Baadhi ya maeneo ya Jiji la Dodoma yamekumbwa na uhaba wa nyama hali inayotishia kupanda kwa bei ya kitoweo hicho.
Hali kadhalika bei ya nguo na vyakula nayo imeanza kupanda tangu wiki mbili zilizopita nakusabisha wananchi wengi kushindwa kumudu kununua mahitaji husika.
Mmoja wa wateja aliyekutwa katika bucha iliyopo Soko la Majengo, John George, alisema kuna uhitaji mkubwa wa nyama ya ng’ombe.
“Nyama kwa sasa imeadimika, sasa ikifika sikukuu yenyewe si tutanunua kwa Sh 10,000 kwa kilo moja?” alihoji George.
Mkazi mwingine wa Dodoma aliyekutwa akinunua nguo za watoto, Shukrani Andrew, alisema bei zimekuwa juu tofauti na mwaka jana.
“Yaani gauni la mtoto wanauza hadi Sh 30,000 wakati nguo za kiume zinauzwa kati ya Sh 40,000 na 45,000. Bora nifanye maandalizi ya watoto kwenda shule tu maana haya mambo ya sikukuu yanatumaliza sana,” alisema Andrew.
Naye mfanyabiashara wa nguo, Emmanuel Ndakidemi, alisema wateja ni wengi na bei hazina tofauti na za mwaka jana.
MTANZANIA pia lilitembelea maeneo yanayouzwa vyakula na kubaini bei za kawaida za mchele kwa kilo ni kati ya Sh 1,800 na 2,500.
Naye Katibu wa Soko la Majengo, Amrani Matimba, akitoa tathmini ya bei ya vyakula katika soko hilo, alisema baadhi ya vyakula vimeanza kupanda bei kama mchele wa Kyela ambao kwa sasa unauzwa Sh 2,500 kwa kilo moja.
Kuhusu uhaba wa nyama alisema hali hiyo inajitokeza kwa sababu wauzaji wengi wanawekeza wakisubiri sikukuu ndipo waanze kuuza kwa bei ya juu.
“Kwa sasa kilo ya nyama ni Sh 6,000 lakini hadi kufikia sikukuu kuna uwezekano ikapanda kufikia Sh 7,000 hadi 8,000 kwa kilo moja,” alisema Matimba.
Alisema pia mafuta ya kula ya alizeti yamepanda bei kwa yanayozalishwa kutoka mkoani Singida ambapo lita tatu yanauzwa Sh 12,000 na lita tano Sh 18,000.
Bei ya kuku nayo imeonekana kuwa juu kwani kuku mmoja alikuwa akiuzwa kati ya Sh 15,000 hadi 30,000 tofauti na siku za nyuma ambapo walikuwa wakiuzwa kati ya Sh 12,000 hadi 18,000.
Comments