Mvua, upepo mkali waleta maafa

KAYA 50 za vijiji vinne vilivyopo Kata ya Ivuna, Tarafa ya Bonde la Kamsamba, Wilaya ya Momba mkoani Songwe wameingia katika hali ya sintofahamu baada ya nyumba zao kuezuliwa na na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa.
Maafa hayo yamesababisha uharibifu wa mazao ya chakula, hivyo kuna hatari familia hizo kukosa chakula na mahali pa kuishi.
Mmoja wa waathirika hao, Difris Sikumbulu alisema mvua iliyonyesha siku mbili mfululizo imesababisha nyumba kuezuliwa na chakula kusombwa na maji.
Alisema kutokana na hali hiyo, hawana uhakika wa chakula na hata uwezo wa fedha kuzijenga upya nyumba zao au kuzikarabati bado ni mtihani, hivyo wanaiomba Serikali na wadau mbalimbali kuwapatia msaada unaowezekana.
Ofisa Tarafa ya Kamsamba, Zakayo Mwasomola alisema maafa hayo yalitokana na mvua kunyesha siku mbili mfululizo ikiyoambatana na upepo.
 Alivitaja vijiji vilivyokumbwa na maafa hayo kuwa ni Mkonko, Samang’ombe, Kasamba na Lwati.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa wilayani humo, Juma Irando, alisema kamati ya wilaya inaendelea kufanya tathimini na kujipanga kuwapatia misaada hiyo.
Irando ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, alisema jitihada za makusudi zinafanyika kuwasaidia waathirika wa maafa hayo, huku akitaja mkakati wa kudumu wa kukabiliana na changamoto ya upepo huo mkali.
Alisema upepo huo mkali umejirudia kwa mara ya tatu tangu ulipoleta madhara ya nyumba 74 kuezuliwa katika Kata ya Ivuna mwaka jana na aliwataka wananchi kupanda miti katika maeneo ya kaya zao ili kupunguza kasi ya upepo unaoweza kusababisha madhara.

Comments

Popular posts from this blog

Wapinzani: Spika tengua kauli yako

Kitakachojiri katika mabasi Des. 20