CCM yatoa neno uhakiki wa taarifa za wakulima wa korosho
Na.Ahmad Mmow,Nachingwea.
Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Nachingwea,mkoa wa Lindi kimeshauri timu ya uhakiki wa taarifa za wakulima wa korosho katika wilaya hii iwe makini ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi.
Ushauri huo ulitolewa jana na katibu wa CCM wa wilaya ya Nachingwea,Rafael Mwita wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya(DCC) kilichofanyika katika mamlaka ya mji mdogo wa Nachingwea.
Mwita ambaye katika kikao hicho alikuwa nimiongoni mwa wajumbe waalikwa,alisema japokuwa uundwaji wa timu hiyo ya uhakiki unania njema ya kutekeleza agizo la Rais kuhusu uhakiki wa taarifa za wakulima wa korosho.Hata hivyo timu hiyo inatakiwa kuwa makini ili kuepuka migongano na malalamiko.
Alisema wakati zoezi hilo linaendelea,tayari zimeanza kutolewa tafsiri tofauti kutokana na kasi ndogo ya malipo ya wakulima wa zao hilo.Ikielezwa kwamba zoezi hilo nimiongoni mwasababu zinazosababisha ucheweshaji malipo.
Aidha Mwita aliishauri timu hiyo kuwa makini kwenye zoezi hilo kwakutambua kuwa wapo watumishi na viongozi wa umma ambao wanamashamba ya korosho.Kwahiyo utumishi wao isiwe sababu ya kuhisiwa na kutiliwa mashaka kwamba wamepata kwa njia zisizo halali.
"Pamoja na nia njema baadhi ya watu wanaweza kuhisi wanaonewa.Kwahiyo umakini unahitajika sana katika kuendesha zoezi hilo,"alionya Mwita.
Mbali na hayo,Mwita alitoa wito kwa serikali kuongeza kasi ya malipo ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wakulima ambao wanataka walipwe,ili fedha hizo ziwasaidie kutatua matatizo mbalimbali.
Kwa upande wake katibu wa timu ya uhakiki,Rafael Ajetu alisema zoezi hilo linakwenda vizuri na timu hiyo inafanya kazi kwa umakini, uangalifu mkubwa na haimpendelei wala kumuonea mtu.Hivyo watu wote waliopata zao hilo kwa njia halali wasiwe na hofu.
Ajetu ambaye pia nimkuu wa idara ya kilimo,umwagiliaji na ushirika wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea alisema hadi sasa wakulima 10,949 wamelipwa.Ambapo shilingi 10.81 bilioni zimetumika kuwalipa wakulima hao.
Katibu huyo watimu ya uhakiki alibainisha kwamba hadi kufikia tarehe 18,mwezi huu,vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS)25 kati ya 39 vilivyopo katika wilaya hii vimehakikiwa.Ambapo vyama 10 kati ya hivyo wakulima wake wamelipwa.Huku taarifa za vyama vitano zimetumwa benki ya kilimo ili wakulima wake waweze kulipwa.
Comments