Marehemu ahukumiwa kwa uhujumu uchumi
ALIYEKUWA Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambaye kwa sasa ni marehemu, Mhandisi Godfrey Majuto, amehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 3.6 na Mahakama ya Wilaya ya Mpanda baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Majuto alifikwa na umauti Desemba 4, mwaka huu wakati akiwa tayari ameshatoa utetezi wake mahakamani hapo.
Hukumu hiyo ilitolewa mahakamani hapo jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Gasper Luoga, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakani hapo na upande wa mashitaka ulioita mashahidi 10.
Mbali na Majuto, washitakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Naomi Nko ambaye wakati huo alikuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Peter Mwanoni, Beatus Bisesa, mkandarasi na Chiyando Matoke.
Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Katavi, Bahati Haule, kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo la kuhujumu uchumi kwa nyakati tofauti.
Alidai walitenda kosa hilo Januari 2, 2012 wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Mpanda wakidai kuandaa hati ya malipo ya uongo ya kutaka kuonyesha sehemu ya Barabara ya Kasokola kwenda Mtapenda kuwa imetengenezwa kwa gharama ya Sh 64,376,152 wakati si kweli.
Katika kosa la pili lililowahusu washitakiwa wa kwanza hadi wa tatu, walishtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi kwa kupitisha malipo hayo kwa Kampuni ya Matoke huku wakijua barabara hiyo haikujengwa kwa gharama hiyo.
Haule alidai kuwa shitaka la tatu liliwahusu washitakiwa wote watano walioshitakiwa kwa kosa la kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya Sh 61,157,342.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili za mashitaka na utetezi, Hakimu Luoga, aliiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa wa kwanza, wa tatu na wa nne wamepatikana na hatia katika kosa la kwanza huku Majuto naye ametiwa hatiani katika kosa la pili na la tatu.
Pia washtakiwa akiwamo wa pili na wa tano hawakutiwa hatiani kwa kosa lolote lile na waliachiwa huru.
Baada ya maelezo hayo, Haule aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa washitakiwa kwa kuwa wameisababishia hasara Serikali.
Akisoma hukumu hiyo, Luoga alisema pamoja na mahakama kupokea hati ya kifo cha Majuto kilichotokea Desemba 4, mwaka huu huko Songea ambako alikuwa akifanya kazi kama Meneja wa Tarura wa Manispaa ya Songea, alikohamia kabla ya mauti hayajamfika alikuwa ameshatoa utetezi wake mahakamani hivyo hakuwa na sababu ya kuifanya mahakama ishindwe kutoa adhabu kwake.
Luoga alisema katika shitaka la kwanza Majuto akiwa na washitakiwa wa tatu na wa nne wamepatikana na hatia ya kifungu cha Sheria namba 22 ya kupambana na rushwa ya mwaka 2007, hivyo wameadhibiwa kulipa faini ya Sh 600,000 kwa kila mmoja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.
Katika kosa la pili na la tatu limemtia hatiani Majuto peke yake na kosa la pili kwa mujibu wa Sheria namba 31 sura namba 11 ya mwaka 2007, amehukumiwa kulipa faini ya Sh 1,000,000 au kifungo cha miaka mitatu jela.
Katika kosa la tatu, Majuto chini ya kifungu cha Sheria namba 57 (1)na kifungu namba 60 (1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, makosa ya kupanga, sura 200, marejeo ya 2002 amehukumiwa kulipa faini ya Sh 2,000,000 au kifungo cha miaka mitano jela.
Hakimu Luoga alisema hukumu hiyo amekukumiwa Majuto na mahakama inaagiza yeyote atakayeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu alipe faini hiyo ili fedha hizo ziende serikalini.
Comments