IMTU yazalisha madaktari 1,478
CHUO cha Kimataifa cha Sayansi ya Tiba na Teknolojia (IMTU), kimefanikiwa kuzalisha madaktari 1,478 na watumishi 2,279 wa sekta ya afya wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini na wengine nje ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Marten Lumbanga, wakati wa mahafali ya 11 ya chuo hicho kwa wahitimu wa shahada ya udaktari na stashahada ya uuguzi.
Lumbanga ambaye ni mjumbe wa bodi ya chuo hicho, alisema ni habari njema kusikia kuwa zaidi ya nusu ya waganga wakuu wa wilaya (DMO) katika maeneo mbalimbali nchini walihitimu IMTU.
“Hii ni habari njema inayotutia moyo hasa kwenu nyinyi wahitimu kwa sababu naamini mtu kupewa nafasi ya DMO lazima aonyeshe uwezo mkubwa wa kitaaluma, uwajibikaji na uhusiano mzuri baina yake na watumishi walio chini yake, wagonjwa na jamii kwa jumla,” alisema.
Kuhusu tishio la Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kufuta usajili wa chuo hicho, Lumbanga alisema IMTU siku zote imekuwa ikishirikiana na TCU kuhakikisha ubora wa elimu wanayotoa.
“Tumepokea kwa mshtuko taarifa za kwamba mnakusudia kutufutia usajili wakati chuo kinaendelea kuboresha miundombinu, walimu na kumbukumbu zinaonyesha kuwa miaka miwili tu iliyopita baada ya TCU kuona jitihada zinazofanywa kuboresha miundombinu ilituruhusu tusajili wanafunzi kwa wingi.
“Kwa maboresho makubwa tuliyoyafanya na tunayoendelea kuyafanya tulitarajia kudahili wanafunzi wengi wapya kwa mwaka wa masomo wa 2018/2019, chuo kisikate tamaa kwa sababu naamini kitaendelea kufanya maboresho na kuwa miongoni mwa vyuo bora vya afya Tanzania,” alisema.
Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kagoma Selemani, alisema kama vyuo vingine chuo hicho nacho kina changamoto nyingi zinazosababisha kisitoe mchango wa kutosha katika ukuaji wa uchumi.
Alisema anaamini IMTU na washirika wake watafanikiwa kukabiliana na changamoto hizo na kuendelea kukua na kuwa miongoni mwa vyuo bora hapa nchini.
Aliwaomba wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa IMTU kila watakakokwenda kufanya kazi na wasisahau kujiendeleza zaidi katika fani zao kwa sababu elimu haina mwisho.
Comments