Kwa Simba Hii, Nkana wajipange upya
WAKATI keshokutwa Jumapili, wakitarajiwa kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Nkana FC ya Zambia, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, ametamba kwamba wanajua umuhimu wa mechi hiyo, hivyo wamejipanga kuhakikisha wanashinda.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji amejinadi kuwa wanataka kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani kushinda lakini lengo kubwa ni kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba wana kibarua cha kupambana na Nkana ya Zambia kwenye mchezo wa marudiano baada ya ule wa awali nchini Zambia kupoteza kwa mabao 2-1, hiyo imemfanya kocha huyo kuelekeza mbinu zake zote katika kutimiza lengo la mchezo wa marudio.
Mbelgiji huyo ameliambia Championi Ijumaa, kwamba amekiandaa kikosi chake na kuwaeleza juu ya umuhimu wa mechi hiyo ambayo imebeba tiketi yao ya kutinga hatua ya makundi lakini ameomba mashabiki waende kuwapa sapoti ya kutosha jambo ambalo litawatoa wapinzani mchezoni.
“Tunafahamu hii ni mechi kubwa na muhimu kwetu, tayari tumejiandaa kikamilifu kabisa kushinda na kupata matokeo mazuri ambayo yatatufanya twende hatua ya makundi, kama mmoja ambavyo amekuwa akitaka hapa kwetu tufike hatua hiyo.
“Tuko tayari kabisa kwa mechi hii na najua tuna uwezo wa kupata matokeo mazuri kwa sababu tunacheza hapa nyumbani, japo hatuwezi kujiamini sana kwa sababu soka lina matokeo yoyote.
“Ninawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani na ikiwezekana hata waujaze uwanja kwa ajili ya kuwapa sapoti wachezaji,” alisema Aussems.
Wakati huohuo, Aussems amemzungumzia beki wake mpya, Zana Oumar Coulibaly baada ya kumpanga kwa mara ya kwanza katika mchezo wa juzi dhidi ya KMC kwa kusema anahitaji muda ili aendane na mfumo wa kikosi chake.
“Nilitaka kukitazama ni namna gani ataweza kufiti kwenye nafasi hiyo, nimpongeze kwani amecheza vizuri japo bado anahitaji muda zaidi wa kufanya vizuri. Hajafika katika kile ambacho nakitaka,” alisema Mbelgiji huyo.
Comments