Mfanyabiashara Akram aachiwa kwa kulipa faini ya sh milioni 259

Na Kulwa Mzee-DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA Akram Azizi aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka 75 ya uhujumu uchumi ikiwamo ya kukutwa na nyara za Serikali, silaha 70, risasi 6,496 na kutakatisha Dola 9,018 za Marekani,  amefutiwa mashtaka baada ya kulipa faini ya Sh milioni 259.
Akramu alifutiwa mashtaka hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kufunguliwa upya mashtaka 73 yakiwamo ya kukutwa na silaha bila kibali, kukutwa na risasi na kilo tano za nyama ya nyati.
Mashtaka mapya yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, akisaidiana na Wakili Simon Wankyo.
Katika mashtaka 75 yaliyofutwa anadaiwa kuyatenda makosa hayo kati ya Juni na Oktoba 30 na 31, mwaka huu katika maeneo ya Oysterbay.
Katika shtaka la kwanza anadaiwa Oktoba 30, mwaka huu maeneo ya Oysterbay alikutwa na meno sita ya tembo yenye thamani ya Sh 103,095,000.
Shtaka la pili anadaiwa Oktoba 30, mwaka huu alikutwa na kilo 65 ya nyama ya nyati zenye thamani ya Dola 1,900 za Marekani bila kuwa na kibali.
Shtaka la tatu hadi shtaka la 72 mshtakiwa anadaiwa kukutwa na silaha mbalimbali aina ya rifle, bastola na shotgun bila kuwa na kibali cha mrajisi wa silaha.
Shtaka la 73 inadaiwa Oktoba 30, mwaka huu mshtakiwa alikutwa na risasi 4,092 na shtaka la 74 alikutwa na risasi 2,404 Oktoba 31, mwaka huu bila kuwa na kibali.
Shtaka la 75, mshtakiwa anashtakiwa kwa kutakatisha Dola 9,018 za Marekani huku akijua ni zao la kosa tangulizi la biashara haramu ya nyara za Serikali pamoja na kukutwa na silaha bila kibali.
Katika mashtaka mapya 73, anadaiwa kati ya Oktoba 30 na 31, mwaka huu alikutwa na silaha 70, nyama ya nyati kilo tano na risasi 6,496 bila kibali.
Mbele ya Hakimu Mashauri mshtakiwa alikiri makosa yote na mahakama ikamtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh milioni 259.
Mahakama hiyo pia iliamuru upande wa Jamhuri kumrejeshea mshtakiwa silaha zote kwa sababu zina leseni na nyingine za watu.
Pia mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo kwa kuzingatia maombi ya Wakili wa utetezi, Agustino Shio, kwamba ni mkosaji wa mara ya kwanza na analiingizia taifa fedha nyingi pia anategemewa na familia.
Upande wa Jamhuri walidai hawana kumbukumbu za makosa ya zamani, mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza.
Mshtakiwa huyo alilipa faini hiyo kwa makosa yote 73 na sasa yuko huru.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja