Tsunami Indonesia:Watu zaidi ya 40 wafariki dunia na 600 kujeruhiwa



Watu zaidi ya 40 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 600 kujeruhiwa kufuatia mawimbi ya tsunami yenye ukubwa wa mita 20 katika Mlango Bahari wa Sunda, ambayo yameharibu pia majumba kadhaa zikiwemo hoteli za kitalii.

Eneo lililoathirika vibaya kwa tsunami hii ni mkoa wa Pandeglang katika jimbo la Banten kwenye kisiwa cha Java, ambacho kina hifadhi ya taifa ya Ujung Kulon na fukwe maarufu, kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Majanga. Katika waliopoteza maisha, 33 wanatokea mkoa huo.

Katika mji wa Bandar Lampung kusini mwa kisiwa cha Sumatra, mamia ya wakaazi walihifadhiwa kwenye jengo la ofisi moja ya serikali.

Mkaazi mmoja wa wilaya ya Pandeglang aliyejitambulisha kwa jina la Alif alisema wimbi la tsunami kwenye eneo lao lilifikia ukubwa wa mita tatu. Alikiambia kituo cha televisheni cha MetroTV kwamba watu wengi walikuwa bado wanawatafuta jamaa zao waliopotea.

"Nililazimika kukimbia wakati wimbi kubwa lilipokiuka ufukwe na kufika umbali wa mita takribani 20 ndani," aliandika Øystein Lund Andersen  kwenye ukurasa wa Facebook. Mtalii huyo alisema alikuwa akipiga picha za volkano alipoona wimbi kubwa likija upande wake.

"Wimbi la pili liliingia hadi ndani ya hoteli niliyokuwa nikikaa na kuzizamisha gari kwenye barabara ya kando yake. Mimi na familia yangu tulifanikiwa kukimbilia maeneo ya juu kupitia msituni na vijijini, ambako tulipokelewa na kuhudumiwa na wenyeji wa hapa. Tunashukuru kwamba hatukuumia," aliandika.

Nyumba 430, hoteli 9 za kifahari zaharibiwa vibaya

Volkano ya Anak Krakatau kwenye Mlango Bahari wa Sunda ambao unaiunganisha Bahari ya Hindi na Bahari ya Java iliripuka dakika 24 kabla ya mawimbi ya tsunami, kwa mujibu wa Mamlaka ya Jiofizikia.

Mbali na vifo vya watu 43, miongoni mwa hasara za mali zilizoorodhesha hadi sasa ni pamoja nyumba 430, hoteli tisa na gari 10 zilizoharibiwa vibaya. Picha zilizotumwa na mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa majanga zilionesha mitaa iliyojaa maji na gari zilizobiruliwa.

Wanasayansi kutoka mamlaka hiyo walisema huenda tsunami hiyo ilisababishwa na maporomoko ya ardhi ya chini ya bahari kutokana na kuripuka kwa kisiwa cha volkano cha Anak Krakatau, ambacho kiliundika miaka kadhaa iliyopita kutokana na volkano ya karibu na kisiwa hicho iitwayo Krakatau.

Sababu nyengine iliyotajwa kuweza kuchochea mawimbi hayo makubwa ya baharini na kupwa na kujaa kwa maji kutokana na mbalamwezi kali.

Mlima huo wa volkano wenye urefu wa mita 305 na ulio umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu wa Indonesia, Jakarta umekuwa ukiripuka tangu mwezi Juni. Mnamo mwezi Julai, mamlaka nchini humo zilitanua wigo wa eneo ambalo halipaswi kutembelea kuwa mzingiro wa kilomita mbili kutoka ulipo mlima wenyewe.

Comments

Popular posts from this blog

KESI YA ZITTO MUSWADA WA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA YAHAMISHWA

Waziri asimamisha likizo za Marubani ATCL