Mama wa watoto nane aamua kugombea urais DRC

Zimebaki siku nne kwa raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kumchagua mtu atakayerithi mikoba ya Joseph Kabila.

Wagombea watatu ndio wanaotajwa zaidi na ni vigumu hata kudhani kuwa wanaowania kiti hicho wapo zaidi ya ishirini na mmoja wao ni mwanamke.

Bi Marie-Josee Ifoku yupo kwenye kinyang'anyiro cha kurithi Ikulu ya Kinshasa kutoka kwa Kabila akichuana na Emmanuel Ramazani, Martin Fayulu na Felix Tshisekedi ambao ndio wanaouvuma zaidi.

Bi Ifoku, mwenye miaka 53 ni mama wa watoto nane si mgeni katika siasa. Alishawahi kuwa naibu gavana wa jimbo la Tshuapa kwa miezi sita mwaka 2016 kabla ya kuchaguliwa kuwa gavana wa jimbo hilo kuanzia Oktoba 2016 mpaka Oktoba 2017.

Mwandishi wa BBC Swahili Mbelechi Msochi amefanya mahojiano na bi Ifoku hivi karibuni na amemueleza mipango yake endapo Wakongomani watampa ridhaa ya kuwaongoza.

Bi Ifoku anasema kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa kufanya mabadiliko ya katiba ili kuhakikisha haki za kiraia zinalindwa na njia ya maendeleo inaandaliwa.

"...kwanza kuwe na mabadiliko kwa upande wa jeshi, polisi pia na uongozi wa kisheria. Tunataka majaji wafanye kazi bila shinikizo, hali itakayowafanya wawekezaji waje wakijua wamehakikishiwa udumishaji wa sheria."

Tatizo la vita limekuwa donda ndugu nchini DRC na bi Ikofu amesema atatumia uwezo wake wote kulishughulikia: "Nataka kuwahakikishia raia wa Congo kuwa mwanamke akichaguliwa kama rais tutahakikisha matatizo kama vita ubakaji na mengineyo yatamalizika. Nitazungumza na nchi jirani juu ya namna gani tutaleta amani."

Comments

Popular posts from this blog

KESI YA ZITTO MUSWADA WA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA YAHAMISHWA

Waziri asimamisha likizo za Marubani ATCL