HapoKale: Wachaga na kisa cha kurudi nyumbani kila mwisho wa mwaka
Wachaga na kisa cha kurudi nyumbani kila mwisho wa mwaka
Kabila la Wachaga linatajwa kuwa la tatu kwa ukubwa nchini Tanzania, ambapo takwimu za mwaka 2003 zinaonyesha kuwa idadi ya Wachaga ni watu 2,000,000.
Shughuli kubwa ya Wachaga ni biashara, kilimo na kazi za ofisini.
“Mangi” ni jina waliloitwa watawala wa Kichaga. Hawa walimiliki mashamba, Ng’ombe na waliheshimiwa kama viongozi wa kikabila. Mangi walikuwa na nguvu za kisiasa na utajiri.
Baadhi ya Mangi mashuhuri katika historia ni Mangi Rindi aliyeingia mikataba na wakoloni (Wajerumani),
Mangi Sina wa Kibosho – anajulikana kwa uhodari wake wa vita katika kupigana na Wamachame na kupora ng’ombe na mazao yao, hata mpaka leo makabila ya Kimachame na Kikibosho hayaoani kwa urahisi, na Mangi Marealle wa Marangu na Vunjo.
Mangi Meli huyu alikuwa Mangi wa wa Oldmoshi ambaye alipigana na Wajerumani na aliishia kukatwa kichwa na mpaka sasa kichwa chake kipo Ujerumani alizikwa kiwiliwili tuu baada ya kumnyonga na mti aliyonyongewa upo mpaka sasa sehemu ya Oldmoshi Bomani karibu na Kolila Sekondari .
Wakoloni walipokuja Kilimanjaro waliingia mikataba na viongozi hawa wa kikabila ili kuweza kuweka misingi yao ya kikoloni. Pia ndugu na watoto wa Ma-mangi walikuwa wa kwanza kupata elimu ya kikoloni, kwa hiyo waliweza kushirikishwa katika Serikali za kwanza.
Hawa pia wanaaminika walikuwa kama mabepari wa kwanza wa kijadi, maana walifanyiwa kazi na watu wengine wakati wao Ma-mangi wamekaa kuhesabu mali zao.
Pia, Wachaga wanatajwa kuwa ni kabila lenye watu wengi zaidi walio na elimu ya kisasa na mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa idadi ya shule za sekondari nchini Tanzania.
Kulingana na takwimu za elimu mkoa wa Kilimanjaro una shule za sekondari zaidi ya 320. Pia mkoa una shule za msingi zipatazo 950. Idadi hii ya shule ni kubwa zaidi ya idadi ya shule katika mikoa mingine Tanzania.
Katika kipindi cha sikukuu hasa za Krismasi na mwaka mpya, Wachaga wengi hupenda kurudi nyumbani, ikiwa ni kuwatembelea wazazi wao, rafiki, au ndugu, wanaukoo kukaa pamoja na kujadiliana mambo jinsi yalivyokwenda katika kipindi kizima cha mwaka.
Pia wakati mwingine katika kipindi hicho Wachaga hutumia muda huo kama sehemu ya kwenda kuwatambulisha watoto kwa bibi na babu zao, hasa wale waliozaliwa mijini.
PATA MAARIFA MENGINE HAPA
Comments