Liverpool yaipasua Arsenal, Firmino achoma kibanda cha bunduki

Liverpool yaipasua Arsenal, Firmino achoma kibanda cha bunduki
Klabu ya Liverpool jana imeipasua Arsenal kwa kipigo cha 5-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza, ushindi ulioiwezesha kujikita zaidi kileleni huku ikitishia usalama wa wapinzani wake.
Arsenal ilikuwa ya kwanza kuchokoza nyavu za Liverpool katika dakika ya 11 baada ya Ainsley Maitland-Niles kupata upenyo na kujikita ndani ya 18 akiwaacha walinzi wa Liverpool kwa mbali. Lakini jua lililoonekana mbele ya Unai Emery halikuwa la machweo bali lilikuwa la alfajiri na kazi ilikuwa inaanza.
Liverpool walijibu dakika tatu baadaye kupitia kwa Roberto Fermito aliyetumia makosa ya safu ya ulinzi ya washika bunduki hao iliyojichanganya. Hata hivyo, Fermito hakuwaacha wanywe maji kwa mshangao wa msawazisho na alipachika goli la pili katika dakika ya 16 ikiwa ni dakika mbili tu tangu ashangilie goli la kwanza.
Mvua ya magoli ilianza kufunguka taratibu dhidi ya Arsenal, ambapo dakika ya 32 Sadio Mane aliwaamsha tena mashabiki wa Liverpool baada ya kuufanyia kazi kwa usahihi mpira aliotengewa na Mohamed Salah.
Makosa ya kumchezea vibaya Mo Salah ndani ya kumi na nane yaliigharimu tena Arsenal baada ya refa wa mchezo huo kumpa penati ambayo alifanikiwa kuipachika nyavuni kwa shuti kali katika dakika ya pili ya nyongeza ya kipindi cha kwanza na kuyafanya matokeo ya nusu hiyo kuwa 4-1.
Kiu ya kujikita zaidi kileleni iliwapa morali Liverpool kuendelea kusaka magoli mengine, ambapo dakika 65 Fermito alilichoma ghala la bunduki kwa kupachika goli la 5 la mkwaju wa penati dhidi ya washika bunduki hao wa Emirates na kufanikiwa kupata hat trick.
Matokeo hayo ni kama Liverpool inatuma salamu kwa Manchester City itakayokabiliana nayo Alhamisi ya wiki ijayo. Kikosi hicho cha Anfield tayari kimeshacheza mechi 20 na kukusanya alama 54 ambazo ni alama 9 mbele ya Tottenham ambayo inawafuatia kwenye msimamo wa Ligi.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja