Udhaifu' wa Bunge wamponza CAG na Mdee
Spika wa Bunge Job Ndugai (Mb) amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad na Mbunge wa Kawe Mhe. Halima Mdee kufika mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kujieleza kufuatia kauli za kudhalilisha Bunge.
Kushoto ni CAG Prof. Mussa Assad, kulia ni Mbunge wa Kawe Halima Mdee
Taarifa iliyotolewa na Mhimilili huo imesema kwamba viongozi hao wamelidhalilisa bunge kwa kuliita kuwa ni dhaifu ambapo Prof. Assad alitoa kauli hiyo akiwa nje ya nchi.
Spika Ndugai ametaka Mussa Assad, CAG afike mwenyewe kwa hiyari yake mbele ya kamati ya maadili ya Bunge tarehe 21. 01.2019 vingenevyo atapelekwa kwa pingu huku Mdee akitakiwa kwenda tarehe 22.
Hivi Karibuni CAG akijibu swali la Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa alisema kitendo cha ofisi yake kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea ni kutokana na "udhaifu wa bunge".
"Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa", alisema Prof. Assad.
Naye Mbunge wa Kawe Halima alimpongeza CAG kwa kitendo hicho ambapo alisema wabunge na mawaziri wa CCM wakiwa nje wanazungumza tofauti na yale ya kwenye Kamera. "Kitendo cha CAG kusema hali siyo nzuri, naimani wanaongoza huu muhimili hawatafikiria kumuita kwenye kamati ya maadili wa kuwa tumekuwa dhaifu, 'Kwa kuwa kweli ni dhaifu", alisema Halima Mdee
Comments