Kigogo mwendokasi, wenzake waachiwa kwa dhamana

Na MWANDIDHI WETU – DAR ES SALAAM
WAFANYAKAZI saba wa Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART), akiwamo kigogo wa idara ya fedha, wanaodaiwa kuhusika katika mtandao wa uhujumu wa mapato ya mabasi ya mwendokasi kwa kuchapisha tiketi feki kwa abiria wameachiwa kwa dhamana.
Hatua hiyo imekuja baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya siku 60 na Jeshi la Polisi huku wakiendelea kusubiri uamuzi wa jalada lao ambalo lipo kwa mwanasheria mkuu wa Serikali, likisubiri hatima yao kama kufikishwa mahakama ama laa.
Pamoja na kuachiwa, wafanyakazi hao ambao awali walikuwa wanane wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi mara kwa mara huku upelelezi wa kesi yao ukiendelea.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema tuhuma zinazowakabili wafanyakazi hao ni za kughushi na kuhujumu mapato ya mradi wa mabasi ya mwendokasi, hivyo upelelezi wake unachukua muda mrefu ili kuhakikisha wanapata mtandao mzima.
Alisema awali Jeshi la Polisi lilikuwa linawashikilia wafanyakazi wanane, lakini upelelezi ulipokuwa unaendelea, walilazimika kuwaongeza wafanyakazi wengine watatu.
“Tumelazimika kuwaachia kwa dhamana kwa sababu upelelezi wa kesi yao bado unaendelea, awali walikuwa wafanyakazi wanne, lakini tumelazimika kuongeza wengine watatu na kufikia saba,” alisema.
Mambosasa alisema jalada la watuhumiwa hao lipo mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili aweze kulikagua na kuangalia taratibu za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikishwa mahakamani.
Alisema upelelezi umechukua muda mrefu kutokana na tuhuma za kughushi zinazowakabili ambazo zimehusisha mtandao wa kihalifu.
Mambosasa alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuwakamata na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kihalifu pamoja na kwenda kinyume na sheria za nchi.

Wafanyakazi wanane wa Udart walikaa mahabusu zaidi ya miezi miwili baada ya kukamatwa wakidaiwa wanajihusisha na mtandao wa tiketi za kughushi huku wengine 18 wakiachiwa kwa dhamana.
Awali, Kamanda Mambosasa alidai kuwa watuhumiwa hao wamefanya kosa la kuhujumu mradi wa Serikali ambao ni wa kitaifa na kimataifa kwa kutaka kufifisha jitihada za Serikali.

“Mradi huu unalitangaza Jiji la Dar es Salaam na taifa kwa ujumla kimataifa, hivyo kwenda kinyume na jitihada hizo za Serikali ni sawa na uhujumu uchumi, upelelezi unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo,” alisema Mambosasa.
Pamoja na hali hiyo, alitoa tahadhari kwa Kampuni ya Udart kuwa makini wakati wa kutoa ajira na kuwataka kufuata vigezo muhimu ili kuepuka kuajiri watu wasiokuwa na sifa.
Gazeti hili katika ripoti yake maalumu iliyochapishwa Juni mwaka huu, kuhusu usafiri wa mabasi hayo, lilifichua namna wajanja wanavyotumia mwanya wa kutokusanya mapato kielektroniki na kusababisha hasara kwa Serikali kukosa mapato yake stahiki.

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa mapato katika Kituo cha Kimara yameshuka kwa kasi kutoka Sh milioni 20 hadi 25 yaliyokuwa yakikusanywa kupitia mfumo wa kielektroniki na kufikia hadi Sh milioni 10 kwa siku.

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, walifanya uchunguzi na kubaini mtandao huo wa wizi huku mmoja wa kigogo wa juu wa kampuni hiyo naye alikamatwa na polisi.
Inadaiwa wafanyakazi hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi (majina yanahifadhiwa kwa sasa kwa sababu za kiuchunguzi), waliunda mtandao maalumu wa kufyatua tiketi feki na kujipatia mamilioni ya fedha.

Mradi huo wakati unaanza mwaka 2016, ulikuwa unabeba abiria 75,000 na kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 200,000.
Kutokana na kila safari abiria hulazimika kulipa Sh 650, ukizidisha kwa idadi hiyo, mapato kwa siku yaliyokuwa yanakusanywa hufikia Sh milioni 130,000 ingawa kwa sasa yameshuka.

Katika mtandao huo imebainika mbali ya kufyatua tiketi feki, pia wamekuwa wakifanya ujanja kwa kuwauzia watu wazima tiketi za wanafunzi Sh 200 badala ya Sh 650 huku kiwango kinachobaki kikiingia katika mifuko ya wajanja.
Aprili 24 na Mei 16, mwaka huu makusanyo yalianza kuhujumiwa baada ya UDART kuingilia kati na kutaka kukusanya wao fedha, huku wakipinga uwepo wa tiketi za kieloktroniki chini ya Kampuni ya Maxcom Afrika Plc.

Hatua hiyo iliifanya UDART kuingilia na kusimamia ukusanyaji wa mapato kupitia tiketi maalumu za mashine huku zikichanwa na wafanyakazi waliowekwa milangoni.
Awali mradi huo ulipoanza suala la makusanyo lilikuwa chini ya Kampuni ya Maxcom Africa ambao walikuwa wakikusanya kielektroniki na kudhibiti wizi huku UDART wakibaki na uendeshaji mabasi.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja