Mshtakiwa adai Waziri Lukuvi alimpora begi la fedha

Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa amedai mahakamani kwamba Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alimkaba akiwa ofisini kwake akimlazimisha kutoa hela alizo nazo kwenye mkoba na alipogoma waziri mwenyewe akafungua zipu akazitoa akaweka mezani na kisha akatoka nje na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakaingia.
Kiluwa amedai hayo leo saa tatu asubuhi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu Mkazi Samweli Obas, akiongozwa na Wakili wake Imani Madega ambapo katika utetezi wake amedai alikuwa kwenye manunuzi ya vitu vya ofisi, walikuwa wanakarabati ofisi, alipanga kuanza kununua kwanza ndiyo aende ofisini kwa waziri lakini Waziri alimpigia simu mara tatu akimuharakisha aende ofisini kwake anamchelewesha ndipo alipokatiza kazi yake akaenda.
Amedai waziri alitaka afike ofisini kwake akiwa na hati zake 57 lakini hakwenda nazo kwa madai kwamba mwenzake anayetunza alisafiri.
“Nilipofika aliniuliza nimebeba nini, nikamjibu nimebeba hela… akasema nipe… nikamwangalia… waziri akainuka ananinyang’anya begi, akanikaba akafungua zipu, akatoa hela akazimwaga mezani, ofisini tulikuwa wawili.
“Sikumpa hela kwa hiari yangu, nataka hela zangu zirudishwe, kusema ukweli waziri anatumika na watu wanaotoka mimi niharibikiwe wao waendelee.
“Waziri anamkwamisha Rais John Magufuli katika azma yake ya kuiingiza Tanzania katika uchumi wa viwanda kwa kujiangalia yeye binafsi,” amedai Kiluwa ambaye anashtakiwa kwa kumpa rushwa ya Sh milioni 90 Waziri Lukuvi.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja