Kwa nini ni msimu wa Liverpool EPL?
IKIWA imetwaa mara 18 taji la Ligi Kuu England, Liverpool ni moja ya klabu ya soka yenye mafanikio makubwa zaidi nchini England.
Hata hivyo, Wekundu hao walitwaa ubingwa wao wa mwisho wakati ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza mwaka 1990, na bado hawajatwaa taji wakati ligi hiyo ilipobadilishwa na kuitwa Ligi Kuu.
Makocha nane tofauti wamejaribu kumaliza ukame wa kutwaa taji hilo kwa Liverpool katika nyakati tofauti, lakini hakuna aliyeweza kufikia mafanikio. Walimaliza nafasi ya pili mara tatu, ukiwamo msimu wa hivi karibuni wa 2013-14.
Hata hivyo, mambo yanaonekana kuwa mazuri kwao msimu huu, kwani wakiwa ndio timu pekee ambayo hadi sasa haijafungwa kwenye Ligi Kuu. Vijana hao wa kocha Jurgen Klopp kwa sasa wapo kileleni mwa msimamo mwa Ligi Kuu na pengine msimu huu anaweza kumaliza ukame huo.
Hapa tunaangalia sababu tatu kwa nini Liverpool itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
3. Safu ya ushambuliaji isiyozuilika
Liverpool ni moja ya timu yenye safu bora zaidi ya ushambuliaji duniani kwa sasa, na ina uwezo wa kuipenya safu yoyote ya ulinzi ya timu pinzani.
Washambuliaji watatu wa mbele wa Wekundu hao kwa pamoja walifunga zaidi ya mabao 90 msimu uliopita, huku Mohamed Salah akitengeneza historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 32 katika mechi 38 za Ligi Kuu kwa msimu mmoja.
Watatu hao pia walianza vizuri msimu huu, na Salah kwa sasa ni mmoja wa wanaoongoza kwa ufungaji kwenye Ligi Kuu akiwa na mabao 10. Sadio Mane na Roberto Firmino pia wako kwenye kiwango kizuri, wakiwa na mabao sita na manne kwa majina yao.
Na hasa ukichukulia ukweli kwamba wote hao wana umri wa miaka 26 na wapo kwenye kiwango cha juu kabisa, Klopp atakuwa anatarajiwa kuiongoza klabu hiyo kutwaa taji lake la kwanza. Uwapo wa Naby Keita unaongoza ubunifu kwa timu hiyo. Pia, Xherdan Shaqiri na Daniel Sturridge wapo pale kama mbadala wa washambuliaji hao watatu wakishindwa kufunga.
2. Safu imara zaidi ya ulinzi
Safu ya ulinzi mara zote ulikuwa ni udhaifu wa Wekundu hao, na imeshuhudiwa mechi nyingi kwa miaka kadhaa, wamekuwa wakicheza vizuri lakini kwenye kuzuia ndio ilikuwa tatizo lao kubwa.
Hata hivyo, usajili wa Virgil van Dijk kutoka Southampton kipindi cha majira ya dirisha dogo Januari kumethibitisha kwamba klabu ilifanya jambo muhimu zaidi, na Mholanzi huyo amekuwa nguzo muhimu zaidi kwenye safu ya ulinzi ya Liverpool na kuwa moja ya timu yenye beki imara zaidi kwa sasa.
Kwa sasa Liverpool ndio yenye safu bora ya ulinzi kwenye Ligi Kuu ya England, kwani imeruhusu kufungwa mabao sita tu katika mechi 16 msimu huu.
Wachezaji kama Joe Gomez, Trent Alexender Arnold, na Andy Robertson wote wamenufaika na uongozi bora wa Van Dijk na wameimarika zaidi tangu kuwasili kwake. Zaidi ni kwamba, Wekundu hao pia walitumia paundi milioni 62 kumsajili Alisson Becker na Mbrazil huyo anafanya kazi yake vizuri.
1. Kutoshuka kiwango
Majogoo hao wamekuwa na kiwango bora zaidi kisishoshuka dhidi ya timu kubwa tangu Klopp awasili klabuni hapo, lakini matokeo ya kuvutia dhidi ya klabu kubwa mara kwa mara yalikuwa yanakatishwa tamaa na yale dhidi ya timu ndogo.
Liverpool ilikuwa inacheza tofauti dhidi ya timu ndogo, kwani ilipokuwa ikikutana na timu kubwa ilikuwa ‘inakaza’. Walipoteza dhidi ya timu zote tatu zilizoshuka daraja msimu uliopita, kitu ambacho kilikuwa kikiiangusha zaidi timu hiyo.
Hata hivyo, mambo yanabadilika msimu huu na Liverpool imeonekana kucheza kwa kiwango kilekile katika kila mchezo unaokuja mbele yao. Liverpool imeshinda mechi 13 kati ya 16 na ndio timu pekee ambayo haijafungwa kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu.
Mafanikio ya kuzifunga timu zote sasa yanaonekana kuibeba Liverpool, kwani kwenye kila mchezo wameonekana kuwa kwenye kiwango kilekile bila kubadilika.
Comments