Kanyasu aagiza tatizo la vinyago litatuliwe


Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
BAADA ya malalamiko ya watalii wengi kulazimika kuacha vinyago viwanja vya ndege walivyokuwa wamevinunua katika maduka mbalimbali nchini kutokana na kukosekana kwa vibali kutoka Wakala wa Huduma za MisituTanzania (TFS), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameuagiza wakala huo uangalie namna bora ya kutatua tatizo hilo kwa kuwa limekuwa na taswira mbaya kwa nchi.
Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipozungumza na watumishi wa wakala huo makao makuu.
Alisema watalii wengi hununua vinyago katika maduka mbalimbali kama zawadi ya kupeleka nchini kwao, lakini wanapofika viwanja vya ndege, hudaiwa vibali vya kuvisafirisha jambo ambalo huwalazimu kuviacha kutokana na usumbufu wanaoupata.
Kanyasu alisema jambo hilo limekuwa likiwafanya watalii wengi kuondoka nchini wakiwa wamekasirishwa kutokana na utaratibu huo kutokuwa wazi, huku wakiamini wamedhulumiwa mali yao.
“Malalamiko hayo si mazuri licha ya kuwa TFS nia yake ni njema ya kuhakikisha lazima kuwe na vibali ya kusafirishia vinyago hivyo kwaajili ya udhibiti wa uharibifu wa misitu,” alisema.
Alisema lazima TFS ifanye mazungumzo na taasisi nyingine ili kutatua kero hiyo ambayo imekuwa ikileta sintofahamu kwa watalii na sekta ya utalii kwa ujumla.
Kanyasu alisema ni rahisi kumpoteza mteja (mtalii), lakini huweza kuchukua hata zaidi ya miaka kumi kuweza kumrudisha mteja ambaye ulikuwa umempoteza.
“Nia ya wakala, ni njema katika kulinda misitu lakini tatizo linaloonekana ni kwamba hakuna mawasiliano thabiti kati ya TFS na taasisi nyingine kuhusu biashara ya vinyago,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja