AZIZA MASOUD – Dar es Salaam MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, amesema hawezi kuungana na vyama vingine vya upinzani vilivyofungua kesi kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018. Amesema anaamini kufanya hivyo hakuwezi kuondoa matatizo yaliyopo ambayo msingi wake unatokana na ubovu wa sheria zilizopo. Mrema ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja kupita baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuanza kusikiliza kesi namba 31 ya kupinga muswada huo iliyofunguliwa mahakamani hapo Desemba 20 mwaka jana na viongozi wa vyama vya upinzani. Viongozi hao ni Kiongozi Mkuu ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Kaimu Katibu Mkuu Cuf (Bara), Joram Bashange na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani. Katika kesi hiyo mshtakiwa mkuu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi. Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake Salasala, Dar es Salaam, Mrema alisema wapinzani wanapaswa kufahamu kuwa hitaji la sasa...