Tumbua tumbua: vigogo Ardhi Kigoma wavuliwa nyadhifa


NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Dk. Angelina Mabula amewavua nyadhifa wakuu wa Idara ya Ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi ipasavyo.
Waliovuliwa nyadhifa hizo ni Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Manispaa ya Kigoma, Brown Nziku, Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Emanuel Magembe na Ofisa Ardhi Mteule, Paul Misuzi.
Mabula alifanya uamuzi huo Januari 3, mwaka huu akiwa mkoani hapa baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Alifikia uamuzi huo baada ya watendaji hao kushindwa kusimamia maagizo na maelekezo yaliyotolewa tangu mwaka juzi kuhusu ukusanyaji wa kodi ya ardhi, uingizaji wa wamiliki wa viwanja na mashamba kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya kielekroniki wa ardhi na utoaji wa hati za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.
Mabula alisema pamoja na barua iliyoandikwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Kanda ya Magharibi, Idrisa Kayera ya Aprili 25, 2017 kwenda kwa watendaji hao na maelekezo aliyoyatoa, lakini bado hawakuonesha umakini katika utekelezaji.
Awali Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ya Kigoma, Emanuel Magembe alitoa maelezo kwa Naibu Waziri, kuwa halmashauri yake kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana ilikusanya Sh. 9,291,400 kati ya milioni 75 ilizopangiwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mathias Kabundugulu, alisema katika kuhakikisha Serikali inapata mapato ya kwenye sekta ya ardhi, jukumu la kwanza ni watendaji wake kuhakikisha mfumo uliopo unatumika ipasavyo pamoja na kupanua wigo wa kukusanya mapato.
Alisema halmashauri ndizo zenye jukumu la kupanga na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ardhi huku wakurugenzi wakipaswa kusimamia ukusanyaji huo na kuwa wabunifu.

Comments

Popular posts from this blog

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC