Waziri Mkuu aibana kampuni inayodaiwa bil 2.9
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza kampuni zote zinazosambaza nguzo za umeme kulipa ushuru wa halmashauri wanakotoa nguzo hizo amboa ni asilimia tano ya gharama ya kila nguzo kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Ametoa agizo hilo jana Jumatatu, Januari 7, 2019 baada ya kupata taarifa kuhusu kampuni ya New Forest ambayo inamkataba na TANESCO wa kusambaza nguzo za umeme, kukaidi kulipa ushuru wa asilimia tano ya gharama ya kila nguzo. Ushuru huo umefikia sh. bilioni 2.9 hali iliyopelekea uongozi wa mkoa kuzuia nguzo hizo zisitoke.
Wiki iliyopita akiwa katika ziara ya mkoa Ruvuma, Waziri Mkuu alipokea malalamiko kuhusu mkoa wa Iringa kuzuia kusambazwa kwa nguzo za umeme ndipo alipoamua kuwaita Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi pamoja na wakuu wa wilaya, wakurugenzi pamoja na wenyeviti wa halmashauri wanaotoka katika wilaya zinazozalisha nguzo.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemevu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Josephat Kandege, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
Baada ya kupata maelezo katika kikao hicho, Waziri Mkuu amemuagiza mkuu wa mkoa wa Iringa kuiandikia bili kampuni ya New Forest ili ilipe ushuru huo kuanzia Julai 2018 walipoanza kusambaza nguzo.
Kampuni hiyo ilizuiwa kutoa nguzo ndani ya mkoa wa Iringa tangu Novemba 2018 hadi Januari 2019 huku ikitakiwa kulipa ushuru wa asilimia tano ya gharama ya kila nguzo ambapo ilikataa ikitaka iendelee kulipa sh. 5,000 kwa kila nguzo kama walivyokubaliana na TANESCO jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Comments