MABURUNGUTU YA PESA MWANZA UTATA WAIBUKA!
MWANZA: Tukio la Jeshi la Polisi jijini Mwanza kukamata kilo 323.6 za dhahabu na maburungutu ya fedha taslim kiasi cha shilingi milioni mia tatu na milioni tano (305,000,000), Jumamosi iliyopita, limeibua sintofahamu na utata mkubwa uliotawaliwa na maswali, Uwazi limedokezwa.
Taarifa za awali zilidai kuwa dhahabu na mamilioni hayo ya shilingi yalikuwa yakisafirishwa kuelekea mkoani Geita. Katika tukio hilo ambalo watuhumiwa watatu wanashikiliwa na jeshi hilo, dhahabu ilikamatwa ndani ya gari katika Kivuko cha Kigongo huku mamilioni hayo yakinaswa ndani ya gari kwenye Kivuko cha Kamanga jijini Mwanza.
Kufuatia matukio hayo mawili, kuliibuka maswali mengi yenye utata na kwamba itakuwa ni miongoni mwa kesi zitakazovuta hisia za wengi kutokana na kiasi hicho kikubwa cha dhahabu na pesa zilizonaswa. “Mimi ninachojua ni kwamba mtu ukitaka kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha lazima uombe ulinzi wa polisi.
“Swali langu ni kwamba ina maana watuhumiwa hao hawakuwa na ulinzi wowote au kibali kwa ajili ya kusafirisha pesa hizo na dhahabu hizo?” Alihoji David Maduhu, mkazi wa Mwanza. Mbali na kuwa au kutokuwa na kibali cha kusafirisha mzigo huo, mwingine alihoji juu ya je, watuhumiwa hao waliruhusiwaje na mamlaka za madini kusafirisha kiasi hicho kikubwa cha dhahabu?
“Mbali na hilo, pia kuambiwa tu kuwa walikuwa wanakwenda Geita haitoshi, watu wanajiuliza huko ndiko kwenye soko la dhahabu? Na mbona bado walikuwa na kiasi hicho kikubwa cha fedha, kilikuwa ni cha nini?”
Alihoji mwananchi mwingine, Charles Gombalo na kuongeza: “Kiukweli hili suala lina utata mkubwa na wengi tungetamani kusikia upande wa pili kwa maana ya watuhumiwa. Tunataka kujua kama hayo mamilioni na dhahabu vilikuwa halali au si halali?
“Katika kipindi tulichonacho cha kulinda rasilimali zetu, ni mtu jasiri pekee anayeweza kufanya kama walivyofanya hawa watuhumiwa na mbaya zaidi kama hiyo dhahabu ilikuwa inasafirishwa bila kulipiwa kodi (6%), basi itakuwa imekula kwao (watuhumiwa) kwani itakuwa ni uhujumu uchumi.”
Wakati sintofahamu hiyo ikitawala, Kaimu Kamanda wa Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Utawala wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Advera Bulimba alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kuwa jeshi hilo litafanya kazi yake kwa uadilifu kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake na watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani mara moja.
Naye Mongela alisema kazi kubwa waliyonayo viongozi wanaosimamia mambo mbalimbali mikoani ni kuhakikisha wanalinda rasilimali za nchi
Comments