SOMA HIYO!:Wananchi wahamasishwa kubangua korosho
HADIJA OMARY-LINDI
MKUU wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga, amewataka wajasiriamali wilayani hapa kuchangamkia fursa ya ubanguaji wa korosho iliyotolewa na Serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Ndemanga aliyasema hayo mjini hapa jana alipokuwa akifunga mafunzo ya ubanguaji bora wa korosho yaliyotolewa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (Sido), Mkoa wa Lindi.
Ndemanga alisema kwamba, Serikali ilipoamua korosho zote zibanguliwe ndani ya nchi, ilikuwa na lengo la kuinua uchumi wa wananchi wake na kwamba wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo ili kuinua uchumi wao.
“Uamuzi wa Sido wa kuwakusanya wajasiriamali na kuwapa mafunzo ya ubanguaji bora wa korosho ni kitendo cha kizalendo kwani kitawafanya wajasiriamali kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya ubanguaji vitakavyowaongezea kipato,” alisema Ndemanga.
Naye Ofisa Uendelezaji Mafunzo kutoka Sido, Aizack Daniely, alisema katika mafunzo hayo ya siku tano yenye lengo la kuongeza kasi ya uongezaji wa thamani katika zao la korosho, jumla ya wajasiriamali 48 wameshiriki kutoka wilaya za Lindi na Nachingwea.
Alisema kwamba, katika mafunzo hayo, washiriki walipata fursa ya kujifunza hatua za ubanguaji bora wa korosho, teknolojia na ubanguaji bora na usalama na afya kiwandani.
Naye Meneja wa Sido, Mkoa wa Lindi, Mwita Kasisi, alisema mafunzo hayo yataendelea kufanyika katika wilaya nyingine kulingana na mahitaji ya wilaya husika.
Aliongeza kwamba, baada ya mafunzo hayo, washiriki wataweza kupata ajira kupitia viwanda vya ubanguaji wa korosho vitakavyofunguliwa na wengine watakwenda kuanzisha viwanda vyao ambavyo vitatoa ajira kwa wananchi wengine.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wabanguaji Wadogo Wadogo, Mkoa wa Lindi, Mariamu Kaisi, alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza kasi ya utendaji kazi tofauti na awali walipokuwa wanabangua korosho hizo kwa mazoea.
Comments