Katibu baraza la ardhi kortini
BENJAMIN MASESE
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita imehukumiwa Katibu wa Baraza la Kata la Nyamboge, Theleza Barnabas, kifungo cha miaka mitano au kulipa sh 200,000 kila kosa kwa kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa.
Alilipa faini na kuachiwa.
Akitoa hukumu, Hakimu wa mahakama hiyo, Jovith Kato alisema mahakama ilizingatia ushahidi wa jamuhuri na ushahidi wa utetezi.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Dennis Lekayo alidai Septemba 13, 2018 katika Kata ya Nyamboge wilayani Geita, mshitakiwa aliomba rushwa ya Sh 200,000 kutoka kwa Sanda Magohe amsaidie kupata ushindi kwenye shauri la ardhi namba 01/2018 dhidi ya Dotto Maonyole lilokuwa linasikilizwa na Baraza la Kata ya Nyamboge.
Baada ya kuombwa rushwa hiyo, Sanda ambaye alikuwa ni mlalamikaji katika shauri hilo, aliamua kutoa taarifa hiyo kwa Takukuru Mkoa wa Geita ambako mtego uliandaliwa kwa kutumia fedha za mtego.
Alisema Septemba 20, 2018 Sanda alimpelekea fedha hiyo mshitakiwa na baada ya kuipokea alitiwa nguvuni na makachero wa Takukuru.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa siku ya kupokea fedha alimwelekeza Sanda wakutane nyumbani kwake na baada ya Maduka kufika kwake mshitakiwa alihoji kama fedha aliyoagizwa imekamilika.
Baada ya kujibiwa kuwa imekamilika, Barnabas alipokea fedha hiyo bila kujua kuwa alikuwa ndani ya mtego wa Takukuru.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Thobias Ndaro alitoa wito kwa wananchi wote wa mkoa huo kuendelea kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa kwa maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla.
Comments