RC Makonda atoa zawadi ya thamani ya sh. milioni 72
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda leo ametoa zawadi ya kufunga mwaka ya Ng'ombe 60 wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 72 kwa Jeshi la Wananchi JWTZ, Jeshi la Polisi, Hospital ya Taifa Muhimbili, Ocean Road na Hospital za Mkoani humo kama chachu ya kuongeza morali ya kazi katika kuwahudumia wananchi.
Katika mgawanyo huo Jeshi la wananchi JWTZ wamepata Ng'ombe 20,Jeshi la Polis Ng'ombe 20 na Sekta ya Afya Ng'ombe 20 ambapo RC Makonda amesema anafurahishwa sana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na vyombo hivyo.
RC Makonda amesema Ng'ombe aliowakabidhi sekta ya Afya wataenda kula Madaktari, Wauguzi na wagonjwa watakaokuwa wodini kwenye hospital zote za Mkoa huo ikiwemo Muhimbili, Ocean road, Amana, Mwananyamala na Temeke ambapo RC Makonda ametoa nyama hiyo Kama zawadi ya sikukuu na pole kwa wagonjwa.
Aidha RC Makonda amevipongeza vyombo vya ulinzi na Usalama kwa kusimamia hali ya usalama jijini humo kuwa shwari masaa 24 na kuwafanya wananchi kuishi kwa amani wakati wote.
Kwa upande wa sekta ya Afya, RC Makonda amesema anajivunia kuona Wananchi wanahudumiwa vizuri tofauti na kipindi cha Nyuma ambacho hospital nyingi za mkoa huo zilikuwa zikigubikwa na kasoro nyingi zilizokuwa zikiwaumiza wananchi.
Pamoja na hayo, RC Makonda amewaomba watumishi wote wa mkoa huo kuongeza uwajibikaji katika kipindi cha mwaka ujao wa 2019 ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri makusanyo ya kodi.
Akipokea zawadi hiyo Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ Meja Jenerali Yakubu Mohamed, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Dr. Grace Maghembe wamemshukuru RC Makonda kwa zawadi hizo na kumuahidi kuongezeka ufanisi katika utendaji kazi.
TAFADHARI WASAIDIE WENGINE
Comments