JPM aibua mapya haya
Rais Dk John Magufuli amebaini siri ya watendaji 100 wa serikali waliokwepa kusafiri ilihali wamekatiwa tiketi za ndege na serikali na amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege nchini (ATCL) kufikia kesho awe amempelekea majina yao ili wakatwe mishahara yao kufidia tiketi hizo.
Akizungumza wakati kuipokea ndege mpya aina ya Airbus A220-300, leo Jumapili Desemba 23, katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam Rais Magufuli amesema imekuwepo tabia ya watendaji wa serikali kusitisha safari zao bila kutoa taarifa yoyote ilihali wameshakatiwa tiketi tayari.
Rais Magufuli amesema hali hiyo ni kero hata kwa abiria wengine kwani wanafika uwanjani wanaambiwa ndege imejaa kumbe haijajaa ila kuna watu walikatiwa tiketi na hawakusafiri.
“Watu wanakatiwa tiketi ila hawasafiri wanakaa kimya hadi muda wa safari unafika ndege iko tupu na inaondoka hivyo hivyo.
“Kufikia kesho niwe nimepewa hayo majina ya watendaji 100 ili walipe fedha za tiketi walizokatiwa na hawakusafiri na watakatwa katika mishahara yao, “ amesema.
Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyakazi wa ATCL kuhakikisha wanafanya kazi kwa ubora wa hali ya juu huku wakijua usafiri wa anga ni huduma lakini ni biashara na ili biashara ikuwe ubunifu unahitajika.
Comments