Rais Magufuli apiga marufuku kuondoa vijiji katika hifadhi
Mwandishi wetu -Dar es Salaam RAIS John Magufuli ameagiza kusitishwa hatua ya kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwamo katika maeneo ya hifadhi. Amewataka viongozi wa wizara zinazohusika kukutana ili kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo. Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli aliagiza viongozi wa wizara husika kubainisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori ama misitu ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima. Pia Rais ameeleza kutofurahishwa kwake na mazao kufekwa kwa kisingizo cha kupandwa ndani ya mita 60 za mito. Alitoa maagizo hayo jana alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangallah, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Joseph Nyamhanga na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika. Kwa...