Mbunge kuwasilisha hoja binafsi lugha ya kufundishia
TIGANYA VINCENT, TABORA
MBUNGE wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM), amesema wakati umefika kwa Watanzania kuanza kutumia Kiswahili kwa ajili ya kufundishia katika shule za sekondari na elimu ya juu kwa masomo yote.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha vijana wengine kuelewa wanachofundishwa na kuwa na ufanisi katika utendaji kazi.
Maige alisema hayo jana mjini Tabora alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hoja yake aliyoiwasilisha bungeni kutaka Kiswahili kitumike kama lugha ya kifundishia na kujifunza katika shule za sekondari na vyuo nchini.
Alisema utafiti uliofanywa na wataalamu na wanazuoni mbalimbali umeonyesha asilimia 50 ya wanafunzi hawaelewi wanachofundishwa kutokana na matumizi ya Kiingereza.
Maige alisema hata wanavyuo vya ufundi wanaofundishwa kwa Kiingereza wanapomaliza masomo yao wanapokuwa kazini hawatumii lugha hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku bali wanatumia Kiswahili.
Mbunge huyo wa Tabora Kaskazini alisema tayari maandalizi ya vitabu vya kufundishia kidato cha kwanza kwa masomo yote vimekamilika pamoja na kamusi kubwa ya tafsiri wa maeneo yote ya Kiswahili iko tayari.
Alisema wataalamu walioandika vitabu hivyo wanasema ikiwa Kiswahili kitaanza kutumia wako tayari kuandaa na vitabu vya kidato cha pili na kuendelea kwa muda mfupi na wanafunzi waanze kuvitumia.
Maige alisisitiza kuwa kwa juhudi hizo za wataalamu hakuna sababu ya kuendelea kutumia lugha ambayo baadhi ya wanafunzi hawaelewi wanachofundishwa.
Alisema hata wananchi wamekuwa wakizielewa zaidi hotuba za Rais Dk. John Magufuli na mijadala ya vikao vya Bunge kwa sababu ya matumizi ya Kiswahili.
Maige alisisitiza kuwa wakati umefika wa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa moyo wake aliouonyesha wa kukiimarisha Kiswahili ndani na nje ya Tanzania anapohutubia mikutano mbalimbali.
Comments