Zuma azua mvutano

4 hours ago Comments Off on Zuma azua mvutano baada ya kupewa msaada wa kurekodi albam yake
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amezua sintofahamu baada ya kupewa msaada na Serikali ya Manispaa kurekodi albam yake ya muziki.
Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya eThekwini kupitia kitengo cha Utamaduni na Urithi imetoa ofa ya kugharamia albam hiyo inayotarajiwa kurekodiwa mwezi Aprili.
Albam hiyo inatarajiwa kuwa na nyimbo ambazo zinazungumzia harakati za ukombozi, mapambano kwenye ulingo wa siasa pamoja na maswahibu yaliyowakuta.
Chama cha upinzani cha Democratic Alliance kimeeleza kuwa kitamuandikia barua Meneja wa eThekwini kumzuia kutumia fedha za umma kwa ajili ya kufadhili kazi za muziki za Zuma.
Diwani wa chama cha Democratic Alliance, Nicole Graham ameeleza kuwa kitengo hicho kilipaswa kutumia fedha hizo kufadhili muziki wa vijana wanaochipukia wanaohitaji msaada na sio kwa mtu mwenye maslahi binafsi ya kisiasa.

“Ni kweli tuna jukumu la kutangaza urithi wetu na kusaidia ukuaji wa utamaduni. Lakini tatizo letu ni pale ambapo manispaa inapoteza fedha kwa ajili ya rais mstaafu ambaye anajaribu bahati yake kwenye kiwanda cha muziki, wakati tuna vijana wadogo wanaochipukia kwenye muziki wanaohitaji msaada,” alisema Ghaham.
Aliongeza kuwa maombi ya kutoa msaada huo kwa Zuma hayakuwasilishwa kwenye kikao cha Halmashauri, kinyume cha taratibu.
Wilaya ya eThekwini iko ndani ya eneo la KwaZulu-Natal ambapo ni nyumbani kwao Zuma na ngome yake kuu ya kisiasa. Zuma hupendelea kuimba wimbo wake maarufu ‘Bring Me My Machine Gun’ akiwa kwenye kampeni.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja