Siasa safi si kuhama chama
LEONARD MANG’OHA
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni imemtangaza mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Mtolea, kuwa Mbunge wa Temeke, nafasi ambayo alikuwa anaishikilia kipindi akiwa mwanachama wa Chama cha Wananchi -CUF .
Tofauti ya ubunge wa sasa na ule aliouvua ni kwamba mara hii amepita bila kupingwa baada ya washindani wake kuondolewa katika kinyang’anyiro hicho kwa kukosa sifa.
Kutokana na washindani hao kukosa sifa NEC, imelazimika kumtangaza kuwa mshindi bila hata kwenda katika masanduku ya kupigia kura, na kutoa haki kwa wananchi kumchagua kiongozi wao wanayemtaka.
Kitendo cha Mtolea kutangazwa na tume hiyo kushika nafasi hiyo bila kupigiwa kura si cha kushangiliwa si tu na wafuasi wa chama chake kipya bali pia yeye mwenyewe, kitendo hicho kinaondoa dhana ya demokrasia na haki ya kuchagua na kuchaguliwa.
Mtolea hapaswi kuufurahia ubunge huo ambao hajautolea jasho. Heshima aliyokuwa nayo awali siamini kama itaendelea kuwa kama alivyopigiwa kura na wananchi wa Temeke mwaka 2015.
Imani ya wananchi anaokwenda kuwaongoza haiwezi kuwa sawa na ilivyokuwa awali. Mtolea anaingi katika orodha ya wabunge na madiwani wengi wa vyama mbalimbali waliovihama vyama vyao na kujiunga na CCM, kwa kile kinachodaiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli katika kuleta maendeleo.
Kwa sababu kuhama chama kimoja cha siasa na kujiunga na kingine ni haki ya kikatiba hawatalaumiwa kwa hilo kwa kuwa wametekeleza haki yao ya kikatiba.
Pia, si kosa kwa mwanachama wa chama kimoja cha siasa kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na kiongozi kutoka chama kingine, hiyondiyo siasa safi inayohubiriwa kwa sababu nia na madhumuni ya walio wengi ni kuliletea Taifa maendeleo.
Kinacholeta maswali miongoni mwa wananchi wengi ni hatua ya wabunge wengi wa upinzani waliovihama vyama vyao kwa hoja ya kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais katika mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa fedha na kuleta maendeleo kwa Taifa.
Binafsi naiona hoja hii kuwa dhaifu kwa kuzingatia kuwa wanaohama vyama vyao wangeweza kuunga mkono juhudi hizo wakiwa huku walikokuwa kwa sababu iko mifano kadhaa baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakimuunga mkono Rais pasi kuvihama vyama vyao.
Naamini kama mtu anamuunga mkono mtu fulani kwa jambo analolifanya ataonekana hata akiwa katika chama pinzani, na hili limejidhihirisha kwa baadhi ya wabunge akiwamo Magdalena Sakaya ambaye Rais mwenyewe kwa maneno yake alipokuwa mkoani Tabora alitamka bayana kuwa licha ya kwamba ni mbunge wa upinzani anatekeleza yale yanayohubiriwa na CCM na amekuwa akiunga mkono.
Hivi karibuni katika uzinduzi wa barabara ya njia nane jijini Dar es Salaam Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, alivyomsifu Dk. Magufuli jinsi anavyotumia kodi za wananchi katika kuwaletea maendeleo kwa kujenga barabara. Hii ndiyo siasa safi na yenye afya kwa Taifa.
Hii ndiyo siasa ambayo wengi tunatamani kuiona, kwa maana kuwa penye kukosoa pakosolewe barabara na penye kuhitaji kusifiwa pasifiwe kwa sababu maendeleo si jambo la upinzani, bali lenye kuhitaji kushirikiana pande zote kwa sababu kila upande unayalenga maendeleo katika jamii na jamii hiyo ndiyo wale wanaowapigia kura.
Naamini mbunge kuunga mkono juhudi akiwa katika chama chake alikopewa ridhaa na wananchi kuna faida kuliko kuhama chama na kuliingiza Taifa katika mzigo mkubwa wa kuandaa uchaguzi ambao unagharimu kiasi kikubwa cha fedha.
Sote tunatambua jinsi ambavyo Rais amekuwa akipambana kubana matumizi hata kwa kufuta matumizi ya fedha kwa baadhi ya mambo yasiyo ya lazima kama vile sherehe za maadhimisho ya Uhuru na kuelekeza fedha hizo katika miradi ya maendeleo ili kuwahakikishia wananchi huduma bora.
Ni lazima wabunge walitazama hili kwa namna ya pekee ili kuokoa fedha zinazotumika kuandaa chaguzi ndogo za marudio zinazotokana na wabunge na madiwani kuvikacha vyama vyao na kujiunga na chama tawala, na wale wanaokihama chama tawala na kujiunga na vyama vingine ama kujivua madaraka na kukaa kando na siasa kama ilivyokuwa aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Ndiyo, ni lazima wabunge kama wawakilishi wa wananchi wamsaidie Rais kuokoa fedha hizi zinazopotea bila sababu ya msingi, kwa sababu bila kufanya hivyo huu utakuwa ni mwanya mwingine wa upotevu wa mapato ya fedha za umma ambazo Rais kupitia Serikali anayoiongoza wamekuwa wakizitafuta kwa kila njia inayowezekana.
Naamini hata Rais mwenyewe hafurahishwi na jambo hili na lingekuwa ndani ya uwezo wake angelitangazia Taifa kuwa mbunge atakayehama jimbo lake litabaki wazi kwa sababu hakuna fedha za kuchezea kwa kufanya chaguzi zisizo za lazima.
Mbali na upotevu, hama hama yenyewe imekuwa si kivutio kwa wananchi walio wengi kwa sababu sisi tunaoishi katika jamii za wananchi wa kawaida tunakutana na maswali, hoja na mijadala inayoonesha wazi kuwa hawafurahii haya yanayofanywa na wawakilishi wao na hilo linaakisiwa kwa idadi ndogo ya wapiga kura wanaojitokeza kupiga kura katika chaguzi hizo.
Matokeo ya vitendo hivi vya dharau kwa wapiga kura dhidi ya wananchi wao waliotumia muda na jasho lao kuwapigia kura linaweza kugeuka mwiba mchungu kwa wabunge wengi waliowasaliti na kuwakwamisha katika uchaguzi Mkuu wa 2020 watakapojitokeza kuwaomba kura.
Si jambo la ajabu tukashuhudia zaidi ya nusu yao wakitupwa nje ya ulingo wa siasa kwa sababu walichokifanya ni kama kuwadharau waliowachagua.
Japo ni haki ya kikatiba kwa mbunge au diwani kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine, ila hama hama hii ya wabunge iliyojitokeza karibuni inaonyesha siasa za kishamba na zisizo na maana yoyote zaidi ya fedheha.
Comments