AJIUA , AMWACHIA MWANAYE BAISKELI !
































BUKOBA: Salvatory Rweyemamu (47) ni baba aliyekuwa mkazi wa Kashai Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ambaye anadaiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kile kilichodaiwa ni hali ngumu ya maisha na kusumbuliwa na ugonjwa kisha kumwachia mwanaye baiskeli kama urithi.  

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Rweyemamu aligundulika kuwa amefariki dunia kwenye chumba chake alichokuwa akiishi katika nyumba ya mwanamke aliyetajwa kwa jina la Tausi Ally.
Ilielezwa kuwa, mwili wa Rweyemamu uligundulika Januari 6, mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi baada ya mtoto wa kaka yake kwenda kumjulia hali. Habari kutoka eneo hilo la tukio zilidai kwamba, mara baada ya kijana huyo kufika nyumbani kwa marehemu Rweyemamu alibisha hodi kwa muda mrefu bila kujibiwa.

Ilielezwa kuwa, baada ya kuona hali hiyo, kijana huyo ilibidi aulizie kwa majirani ndipo majirani hao na rafiki wa marehemu, Andrew John walipochungulia kwa dirishani na kugundua mwili wa Rweyemamu ulikuwa ukininginia kwenye dari. Ilidaiwa kuwa, kutokana na hali hiyo taarifa zilitolewa kwa mwenyekiti wa kijiji hicho, Victor Herman ambaye alifika eneo la tukio kisha aliwajulisha polisi ambao nao waliwasili eneo hilo.
“Baada ya polisi kufika waliuteremsha mwili wa Rweyemamu kutoka kwenye kitanzi na katika kupekuapekua chumbani ndipo wakakutana na ujumbe,” alisema mmoja wa mashuhuda hao. Ilifahamika kuwa ujumbe huo ulisomeka;

“Nimeamua kujiua, maisha yamekuwa magumu, ….(anataja ugonjwa) ni noma, baiskeli yangu ipo kwa fundi apewe mwanangu.” Kwa upande wake, mdogo wa marehemu, Bernadetha Rweyemamu (30), kwa masikitiko makubwa alisimulia kuhusu msiba wa kaka yake.

Alisema kuwa, kwa wiki tatu zilizopita, kaka yake alikuwa akijihisi kuumwa mara kwa mara na baada ya kupimwa, aligundulika kuwa na ugonjwa wa…. (anautaja), hali iliyomfanya aanze kuzorota kiafya na kuwa mtu wa mawazo sana. Alisema kuwa, kwa kipindi chote hicho hadi umauti unamfika, Rweyemamu alikuwa akiishi peke yake huku akiendelea na shughuli zake za kila siku za uchomeleaji vyuma.
Kwa upande wake rafiki wa marehemu, Andrew alisimulia; “Rweyemamu alikuwa na rafiki yake na walifanya shughuli zao pamoja katika karakana yao ya uchomeleaji. “Kwa mara ya mwisho waliachana wiki iliyopita akiwa katika hali ya kawaida kama siku zote isipokuwa alionekana mwenye mawazo sana.”

Naye Denice James (27) ambaye ni jirani wa marehemu alisema; “Marehemu Rweyemamu (Babu) alikuwa mtu wa kujifungia ndani muda mrefu na wakati mwingine alikuwa anajifungia kwa siku hata tatu bila kutoka nje ingawa aliishi kwa ushirikiano mzuri na majirani zake.”

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, mwili wa marehemu ulihifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Bukoba kusubiri taratibu za mazishi. Rweyemamu ameacha mke na watoto watatu huku akisisitiza baiskeli yake iliyokuwa kwa fundi apewe mwanaye.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja