JPM afyekelea mbali maelekezo mapya wimbo wa taifa, bendera
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli, ameagiza bendera, nembo na wimbo wa taifa viendelee kutumika kama awali na kufuta maelekezo yalitolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, katika barua yake iliyoelekezwa kwa vyuo na taasisi za serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, leo Ijumaa Desemba 14, barua hiyo imetoa maelezo ambayo yanaathiri uzalendo wa Watanzania na imeleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo katika bendera ya taifa.
“Hata mimi mwenyewe tangu nasoma shule hadi leo nafahamu kuwa Bendera ya Taifa ina rangi ya njano na si rangi ya dhahabu na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote, sio dhahabu peke yake.
“Kwa hiyo nimeamua kufuta barua kama kuna mabadiliko basi ni lazima yafanyike kwa kuzingatia taratibu zote kwa kuwa jambo hili ni la kitaifa, si la mtu mmoja,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwa wazalendo, kupenda nchi yao na kuitangaza popote walipo ili mradi wanazingatia sheria na maslahi mapana ya Taifa.
Comments