Naibu Waziri aiagiza Tanesco kufikisha umeme Vituo 300 vya afya nchini

Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu katika kuumga mkono Juhudi za Rais Dk . John Pombe Magufuli ya kuboresha sekta ya afya hapa nchini ameliagiza Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wanapeleka miundombinu ya nishati ya umeme haraka iwezekanavyo katika maeneo ya vituo vipya vya afya 300 pamoja na hospitali 69 ambazo zinajengwa na serikali kwa lengo la kuboresha huduma ya matibabu kwa wananchi wake.

Mgalu ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu kupitia Mkoa wa Pwani alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo iliyopo katika halmashauri ya mji Kibaha pamoja na kukagua mwenendo wa ujenzi wa upanuzi katika kituo cha afya mkoani kilichopo Wilayani Kibaha.

“Kwa kweli nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inafikisha kwa haraka miundombinu ya umeme katika vituo vipya vya afya ambavyo vinajengwa pamoja na hospitali hivyo nachukua nafasi hii kuwaagiza Tanesco pamoja na REA kufikisha umeme haraka iwezekanavyo katika maeneo hayo ili wananchi waweze kupata huduma ya afya katika mazingira ambayo ni rafiki kwao na katika hili tunamshukuru sana Rais wetu Dk. John Pombe Magufuli,”alisema Mgalu.

Aidha alibainisha kwamba kwa sasa lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inaboresha miundombinu ya umeme katika maeneo mbali mbali ili zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ziweze kupata nishati ya umeme wa uhakika ambao utasaidia kuboresha zaidi katika utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa Tanzania ambao hapo awali walikuwa wanateseka.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa halmashauri ya mji Kibaha Tulitweni Mwinuka alisema kwamba wamepokea kiasi cha shilingi milioni 500 kutoka serikali kuu kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho cha afya mkoani katika maeneo ya wodi ya wazazi,jengo la mionzi jengo maalumu kwa ajili ya kufulia pamoja na jengo la upasuaji ambapo kukamilika kwake kutaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya mlundikano kwa wagonjwa.

Nao baadhi ya wanawake Wilayani Kibaha Elina Mngonja na Selina Wilsoni wamemshukuru Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli kwa kuboresha sekta ya afya hapa nchni ambapo wamesema kukamilika kwa upanuzi wa kituo hicho hasa katika wodi za kinamama wajawazito utakuwa ni mkombozi mkubwa katika suala zima la utoaji wa huduma hasa wakati wanapokwenda kujifungua.

Comments

Popular posts from this blog

KESI YA ZITTO MUSWADA WA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA YAHAMISHWA

Waziri asimamisha likizo za Marubani ATCL