Makubwa yawakumba Vigogo Tanesco

Ni kutokana na katikakatika umeme
MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameagiza kung’olewa kwa vigogo wawili wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwa kile alichodai ni sababu ya uzembe.
Mbali ya kung’olewa, Waziri Kalemani ameagiza vigogo wavuliwe nyadhifa zao zote na uchunguzi wa kina dhidi yao uanze mara moja.
Dk. Kalemani alitoa maagizo hayo mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Dk. Alexander Kyaruzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma juzi, Dk. Kalemani aliwataja vigogo hao ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji, Mhandisi Abdallah Ikwasi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji,Mhandisi Kahitwa Bashaija.
“Kwa hiyo kuanzia sasa bodii chukue hatua dhidi ya Naibu Mkurugenzi wa ‘Generation’ (uzalishaji umeme) na Naibu Mkurugenzi wa ‘Transmission’ (usambazaji umeme).
“Bodi ichukue hatua za kiutawala ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa zao kuanzia leo (juzi) na uchunguzi wa kinaufanyike kwa mamlaka mliyonayo,” alisema.
Dk. Kalemani alisema amefikia hatua hiyo kutokana na kukatika kwa umeme kulikotokea juzi na kusababisha nchi kukosa nishati hiyo kwa muda wa nusu saa.
Alisema kutokana na taarifa za kukatika umeme na kuyumba kwa usambazaji kutoka gridi ya taifa, viongozi hao wameshindwa kuchukua hatua.
Alitoa maagizo mazito akitaka matatizo ya umeme yamalizwe haraka na baadhi ya watendaji wa shirika hilo ambao si waaminifu au wazalendo wawajibishwe kuanzia juzi.
Alisema nia yake ya kuwaita viongozi wa bodi ya shirika hilo Dodoma, ni kusisitiza maagizo hayo yanatakiwa kuanza kutekelezwa tangu alipoitisha kikao hicho.
“Nimewaita bodi kuja kuwapa maelekezo yafuatayo; maelekezo ya kwanza lazima bodi ichukue hatua kuanzia sasa, hakikisheni kinachosemwa kuhusu gridi kutoka, gridi haitoki na kusababisha nchi nzima au sehemu ya nchi kukosa umeme, lazima bodi ichukue hatua za makusudi kuhakikisha hilo halijitokezi tena.
“Maelekezo yangu, mwenyekiti wa bodi na menejimeti yako unda tume mahususi kuanzia leo (juzi), ya kuchunguza na kufuatilia jambo hili kwa kuhusisha tasnia na taasisi mbalimbali, siyo kutoka ndani ya Tanesco pekee. Ndani ya siku saba nipate matokeo ya nini chanzo cha tatizo hili ili lisijirudie kabisa,” alisema.
Dk. Kalemani alisema maelekezo ya pili kwa bodi hiyo ni kuwa hadi tatizo kama hilo linatokea, ni kwamba kunauzembe katika usimamizi au kutokufuatilia maelekezo ya Serikali, au kunawezakuwa na hujuma kutoka kwa baadhi ya watumishi wasiokuwa wazalendo.
“Kwahiyo kuanzia sasa bodi ichukue hatua dhidi ya Naibu Mkurugenzi wa ‘Generation’ na Naibu Mkurugenzi wa ‘Transmission’. Bodi ichukue hatua za kiutawala ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa zao kuanzia leo.
“Naomba nirudie katika hili la pili, ni kwamba bodi lazima ichukue hatua mahususi dhidi ya Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha ‘Generation’ na Naibu Mkurugenzi wa ‘Transmission’ kuanzia sasa, ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa zao.
“Haya yanatokana na uzembe wa kutochukua hatua za kuwawajibisha watu wa chini yao. Jambo hili limejitokeza mara nyingi sana. Haiwezekani nchi ibaki kwenye giza kwa nusu saa maana yake usalama wa nchi haupo.
“Haiwezekani nchi viwanda visimame kwa nusu saa. Maana yake uzalishaji unasimama na kodi ya Serikali inapotea. Hawa watu waanze kuchunguzwa mara moja pamoja na wote wanaohusika,” alisisitiza.
Agizo la tatu, alisema bodi ihakikishe maeneo yote ya mjini ambayo hayana umeme kwa sasa na yanasubiri kuunganishiwa umeme kupitia shirika yanaanza kuunganishiwa kuanzia sasa ndani ya miezi mitatu.
“Hii ni kazi yako mwenyekiti wa bodi, toa maelekezo kwa menejimenti yako,” alisema.
Alieleza yapo maeneo ya mijini ambayo yanahitaji kuunganishiwa umeme, lakini yamekaa bila umeme kwa muda mrefu na yako ndani ya mipango ya shirika na fedha zimeshatolewa kila mkoa, hivyo Serikali inahitaji kuona yanaunganishiwa umeme ndani ya miezi mitatu.
“Agizo la nne, wateja wote ambao wameshalipia bili zao, wengine wana miezi miwili, wengine mwezi mmoja, wengine miezi mitatu, waunganishiwe umeme nchi nzima ifikapo tarehe 31 mwezi huu. Haya ndiyo maelekezo mahususi ambayo nimewaita niwape ili yaanze kufanyiwa kazi.
“Katika hili, mwenyekiti mchunguze na kuongeza mambo mengine mnayoona yanafaa ili kuhakikisha ustahimilivu wa umeme katika nchi yetu unaendelea.
“Tuhakikishe maeneo yote hayakatiki umeme bila sababu. Matengenezo yanapofanyika wananchi wapewe taarifa, lakini wapewe pia taarifa ni kwa muda gani yanakamilika.
“Mwenyekiti wa Bodi nikuombe sana, chukua hatua za kiutawala dhidi ya watumishi wengine wa shirika wenye dalili za kuhujumu miundombinu ya shirika kadiri utakavyoona inafaa,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog

Wanakijiji watishia kumburuza kortini DC

TMA yatoa tahadhari mafuriko yaja