Ndugai Tundu Lissu, ‘Unatakiwa urudi haraka’
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemtaka Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu kurejea nyumbani kwa kuwa hana kibali cha kuwa nje ya nchi.
Ndugai amesema kuwa hawezi kumpangia Lissu mambo ya kusema ila ajue hana kibali cha kuendelea kuwa nje ya nchi wakati ofisi ya Spika haina taarifa.
“Yeye ametoka kuugua aache uzushi arudi nyumbani, tunamsubiri nyumbani, kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura, sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake, asimpe sababu,”amesema Ndugai.
Aidha, Lissu ambaye amepona majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mwaka juzi, amedai kigezo kinachotaka kutumika kumvua ubunge ni utoro bungeni, ametoa waraka aliouita ‘Baada ya risasi kushindwa, sasa wanataka kunivua Ubunge’.
Aidha, Lissu ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii kuwa, ”Ni taarifa gani ya maandishi watu hawa wanahitaji wakati nilishambuliwa nikiwa kwenye vikao vya Bunge Dodoma. Wakati wote ambao nimekuwa kwenye matibabu uongozi wa Bunge umewasiliana kwa maandishi na mwakilishi wa familia yangu kuhusu matibabu yangu. Wametoa matamko mengi hadharani kuhusu kushambuliwa kwangu na kuhusu matibabu yangu,”
Hata hivyo, Lissu ambaye amemaliza matibabu yake nchini Ubelgiji na sasa anafanya ziara katika nchi za Ulaya amedai kuwa kuna mkakati wa kumvua ubunge akidai Bunge nalo linashiriki katika mpango huo.
Comments