Ubelgji yakubali kumpa hifadi Gbagbo
BLUSSELS,Ubelgji
SERIKALI ya hapa imekubali kumpa hifadhi kiongozi wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, wakati akisubiri matokeo ya rufaa iliyokatwa kupinga kuachiwa na Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia Makosa ya Uhalifu wa Kivita ICC iliyopo mjini The Hague nchini Uholanzi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Januari 15 mwaka huu Mahakama hiyo kumwachia Gbagbo na msaidizi wake, Charles Ble Goude,baada ya kuwafutia mashtaka ya kuhusika na ghasia zilizolipuka katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika mwaka 2010.
Baada ya kufikia uamuzi huo, kesho yake mahakama hiyo ikaeleza kuwa haioni sababu ya kuendelea kumshikilia mahabusu na hivyo ikasema kuwa inaweza kumkabidhi kwa nchi ambayo itakuwa tayari kumpokea.
“Kulikuwa na ombi kutoka mahakamani la kumpa hifadhi Gbagbo na hiyo ilikuwa kazi rahisi kwa sababu ana familia nchini Ubelgji kwani mkewe na wanawe wanaishi Brussels,” Waziri wa Mambo ya Nje wa hapa, Didier Reynders alikiambia kituo cha televisheni ya umma RTBF.
“Tulifikia makubaliano kwamba ni sahihi akaishi Ubelgji, baada ya kuachiwa kwa masharti,”aliongeza waziri huyo na kuongeza kwamba masharti mengine ya kuishi nchini humo watajadiliana na ICC likiwamo la matembezi ya Gbagbo,” alisema.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya hapa mmoja kati ya wake za Gbagbo mwenye umri wa miaka 47, Nady Bamba anaishi mjini hapa.
Katika kesi hiyo waendesha mashitaka wanasema kwamba watakata rufaa kupinga hukumu hiyo ya Januari 15 mwaka huu, lakini wanachokisubiri ni kupata nyaraka za hukumu hiyo ya majaji ili waweze kuamua jinsi ya kuanza mchakato huo.
“Kitu pekee tuna nafasi ya kupitia kwa umakini sababu zilizosababisha kuachiwa kwake na hapo ndipo ofisi yangu itaweza kukataa rufaa,” alisema Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda.
Kwa upande wake wakili wa Ble Goude, alisema kwamba bado wanasubiri nchi ambayo itakuwa tayari kumuhifadhi.
Comments