Wanafunzi 133, 000 waliofaulu, wakosa madarasa sekondari
WANAFUNZI 133,747 sawa na asilimia 18.24 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali kwamwaka 2019 kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Akizungumza jana Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Seriklali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo alisema wizara hiyo imekamilisha zoezi la uchaguzi wa wanafunzi wanaopaswa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ambapo jumla ya wanafunzi 599,356 sawana asilimia 81.76 wamechaguliwa kati ya733,103 waliofaulu.
“Aidha jumla ya wanafunzi 133,747 sawa na asilimia na asilimia 18.24 ya waliofaulu hawakupata nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa,”alisema Jafo.
Jafo alitaja mikoa 17 ambayo ina uhaba wa vyumba vya madarasa na idadi ya wanafunzi waliobaki ni pamoja na Arusha wamebaki wanafunzi 18, 719, Dodoma wanafunzi 5, 991, Iringa wanafunzi 2,774 , Kagera wanafunzi 14, 046, Kigoma wanafunzi 12, 178,Lindi wanafunzi 1, 294.
“Mikoa mingine ni Mara wanafunzi 16, 365, Mbeya wanafunzi 6, 395,Pwani wanafunzi 4, 731, Rukwa wanafunzi 4 ,93, Tabora wanafunzi 11, 209, Tanga wanafunzi 5, 400, Manyara wanafunzi 5, 392, Shinyanga wanafunzi 6,271, Katavi wanafunzi 1, 249, Njombe wanafunzi 3, 172 na Simiyu wanafunzi 12, 684, ”alisema Jafo.
Kutokana na hali hiyo Jafo aliziagiza halmashauri na mikoa iliyobakiza wanafunzi waliofaulu kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwawezesha wanafunzi hao kujiunga na kidato cha kwanza kabla ya Februari mwakani.
Aidha mikoa tisa imeweza kuwachagua wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Kilimanjaro, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Singida na Songwe.
Jafo amewaagiza wakuu wa mikoana wilaya kusimamia mapokezi ya wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji shuleni ili kubaini changamoto mbalimbali na hatimaye kutatuliwa haraka.
Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa shule za Tanzania Bara ulifanyika Septemba tano na sita mwaka huu ambapo jumla ya watahiniwa 960, 202 kutoka katika shule 16, 845 walisajiliwa kufanya mtihani huo.
Likitangaza matokeo mtihani huo, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), lilisema ongezeko la ufaulu ni asilimia 4.76% tofauti na ufaulu wa 2017 ambao ulikuwa asilimia 72.76%.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, alisema katika tathmini ya awali kiwango cha ufaulu kimepanda kwa asilimia 4.9% ikilinganishwa na 2017, amesema pia kiwango cha ufaulu wa somo la Kiingereza uko chini sana tofauti na masomo mengine (50%).
NECTA pia limewafutia matokeo watahiniwa 357 waliobainika kufanya udanganyifu kwenye mitihani iliyofanyika mwaka huu 2018.
“Baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa zaidi 100 kutokana na kuugua kipindi cha mtihani na kuwapa fursa ya kufanya mtihani huo mwaka 2019,” alisema Msonde.
Comments